Ufasiri Kipragmatiki Wa Diskosi Katika Gazeti La Taifa Leo Juu Ya Uhifadhi Wa Misitu Kenya
Abstract/ Overview
IKISIRI
Matumizi ya mikakati mbalimbali ya kipragmatiki katika diskosi huweza kuzua utata katika
kufasiri ujumbe ulionuiwa kumfikia msomaji au msikilizaji. Tamko la msemaji au
mwandishi fulani huweza kufasiriwa na msikilizaji au msomaji kwa njia mbalimbali. Hali
kama hii huibua maana mbalimbali za ujumbe mmoja ambapo mawasiliano hutatizika.
Utafiti huu ulinuia kubaini jinsi mikakati ya kipragmatiki inavyodhihirika katika diskosi za
uhifadhi wa misitu katika gazeti la Taifa Leo nchini Kenya. Vile vile utafiti huu ulinuia
kuonyesha j insi mikakati hiyo inavyoathiri ufasiri wa ujumbe unaodhamiriwa na mwandishi
hivyo basi kutatiza juhudi za serikali za kuhifadhi misitu. Malengo ya utafiti huu yalikuwa:
Kubaini mikakati ya kipragmatiki inayotumiwa katika diskosi za uhifadhi wa misitu ili
kupitisha ujumbe ulionuiwa na mwandishi, kujadili njia mbalimbali zinazotumiwa na umma
kufasiri maana katika habari juu ya uhifadhi wa misitu na mwisho, kueleza athari ya ufasiri
wa kipragmatiki wa habari juu ya uhifadhi wa misitu kwa shughuli za uhifadhi wa misitu.
Nadharia ya kipragmatiki ya 'umaanishi wa kimaongezi' ya Grice ilituongoza katika utafiti
huu. Data kuhusu mikakati mbalimbali ya kipragmatiki katika diskosi ya uhifadhi wa misitu
ilikusanywa kwa njia ya uchanganuzi wa yaliyomo ambapo nakala zote 36 za magazeti ya
Taifa Leo ya mwaka baina ya 2008 na 2009 zilihusishwa. Mikakati mbalimbali ya
kipragmatiki kama vile, matumizi ya jazanda,· kinaya, umaanisho, semi, vionyeshi na
matumizi ya uongo ilibainishwa. Hojaji iliyotayarishwa na mtafiti kwa kuzingatia mada ya
utafiti huu ilitumiwa kukusanya data kutoka kwa umma. Jumla ya watu wazima 50 wenye
umri wa miaka 18 na zaidi na wanaojua kusoma na kuandika kutoka katika eneo la Msitu wa
Kakamega haswa kata za Lukusi, Ivihiga, Kambiri na Lubao waliokuwa wakihudhuria
mabaraza ya chifu walijitokeza kuhojiwa. Wahojiwa hao walipokezwa hojaji ambapo
walizijaza kwa kuzingatia maswali yaliyokuwa yameulizwa. Aidha utafiti huu ulidhihirisha
kuwa matumizi ya kinaya na jazanda katika habari juu ya uhifadhi wa misitu ndiyo
husababisha ufasiri uliopotoka wa kiwango cha juu zaidi-asilimia 64% na 42% mtawalia.
Utafiti huu vilevile ulidhihirisha kuwa ufasiri wa kipragmatiki wa habari juu ya uhifadhi wa
misitu na umma una athari hasi katika shughuli za uhifadhi wa misitu. Kutokana na matokeo
ya utafiti huu mapendekezo yafuatayo yalitolewa: Uhariri wa habari zinazochapishwa katika
gazeti la Taifa Leo juu ya uhifadhi wa misitu ufanywe kwa misingi ya kuhakikisha kuwa
utata wa ufasiri wa habari unaotokana na kuwepo kwa mikakati ya kipragmatiki
umepunguzwa kabisa kama sio kuondolewa.