Uhusika katika mashairi ya Kiswahili: Malenga wa vumba, Kichomi na Utenzi wa Fumo Liyongo
Abstract/ Overview
Uhusika katika ushairi wa Kiswahili ni kipengele ambacho hakitiliwi maanani na wahakiki wengi wa mashairi. Uhusika huu haujitokezi wazi kama ilivyo katika tanzu zingine za fasihi. Aghalabu huwa si dhahiri, huonekana kuwa tata kutokana na umbo na muundo wa utanzu huu. Uhusika katika ushairi upo ila hubainika kupitia vipengele vingine. Suala kuu la utafiti wetu ni vipengele vinavyodhihirisha uwepo wa uhusika katika ushairi wa Kiswahili. Azma ilikuwa kutathmini uhusika na usawiri wa wahusika mbalimbali kama wanavyojitokeza katika mashairi ya Kiswahili. Madhumuni ya utafiti huu yalikuwa ni: Kutathmini jinsi uhusika unavyojitokeza katika ushairi wa Kiswahili, kubainisha aina za uhusika katika mashairi ya Kiswahili na kuchunguza usawiri wa wahusika katika ushairi wa Kiswahili. Upeo wa utafiti huu ni uhusika katika ushairi kwa kurejelea diwani mbili na utenzi mmoja. Hivyo basi upeo wa mada ni usawiri wa uhusika katika tanzu tofauti za mashairi. Utafiti uliongozwa na Nadharia ya Usimulizi kwa mujibu wa Manfred (2005). Mihimili mikuu ya nadharia hii ni dhana ya uhusika na usimulizi. Kwa mujibu wa nadharia hii suala la kimsingi ni kutathmini ni nani mrejelewa, anachukuwa sehemu ya nani, akiwa kama nani. Utafiti ulichukua muundo wa kiuchanganuzi. Data iliyokusanywa ilitathminiwa kimaelezo. Mbinu za ukusanyaji data zilikuwa unukuzi na uchunzaji kupitia orodha ya uchunzaji. Sampuli dhamirifu ilitumika kuteua diwani ya Malenga wa Vumba (1981), diwani ya Kichomi (1974) na Utenzi wa Fumo Liyongo (1973) kutoka Afrika Mashariki. Usampulishaji huu ulitumika kwa sababu ulilenga tungo mahsusi, hivyo basi ufafanuzi mwafaka kutolewa kuhusu uhusika. Data iliyokusanywa ilifafanuliwa kwa kina kwa kuegemea dhana ya uhusika. Matokeo ya uchunguzi yamedhihirisha kwamba uhusika katika ushairi upo kwa kuwa mashairi hutungwa kutokana na mazingira anamoishi mtunzi na siyo kutoka kwenye ombwe. Utafiti unatoa mchango kuhusu suala la uhusika katika ushairi na fasihi kwa jumla. Utafiti huu ni miongoni mwa tafiti chache ambazo zimefanywa kuhusu uhusika katika ushairi wa Kiswahili. Aidha utawafaidisha wasomi wengi wakiwemo wahadhiri, walimu na wanafunzi wanaotafuta uelewa wa ushairi wa Kiswahili. Utafiti huu utawafaa wahakiki wengi wa fasihi ya Kiswahili. Utafiti unapendekeza utafiti linganishi wa wahusika katika ushairi na tanzu zingine za fasihi ya Kiswahili.