Uhakiki wa suala la uhifadhi wa mazingira katika tanzu teule za fasihi ya kiswahili ya milenia mpya
Abstract/ Overview
Hatua nyingi madhubuti zinachukuliwa na wanafasihi na mashirika mbalimbali kuhamasisha binadamu juu ya masuala yanayohusiana na uharibifu wa mazingira pamoja na haja ya uhifadhi wa mazingira. Hii ni kwa sababu wanadamu katika milenia mpya wamekumbwa na vitisho vya maangamizi kutokana na uharibifu na kuzorota kwa mazingira. Fasihi imechangia kutoa suluhu kwa tatizo hili. Hata hivyo, mchango wa fasihi ya Kiswahili katika mchakato huu haujaangaziwa. Utafiti huu uliazimia kubaini vile fasihi ya Kiswahili ya milenia mpya inavyoweza kutumika kuangazia hali hii. Utafiti uliongozwa na lengo kuu ambalo ni kuchunguza kazi za kifasihi za milenia mpya za Kiswahili kwa mtazamo wa uhakiki kimazingira. Madhumuni ya utafiti huu ni: Kubainisha masuala ya kimazingira katika tanzu teule za fasihi ya Kiswahili ya milenia mpya; kujadili athari kuhusu masuala ya mazingira kama zinavyojitokeza katika tanzu teule tatu za fasihi ya Kiswahili; kutathmini mchango wa fasihi ya Kiswahili katika uhifadhi mazingira. Nadharia ya Uhakiki-Kimazingira iliyoendelezwa na Glotfelty na Fromm (1996) ilitumika na mihimili yake ya tabia ya binadamu, utamaduni na lugha ya msanii kuoana na mazingira ilikuwa amilifu katika uchanganuzi wa matini ya utafiti. Muundo-elezi kupitia uchanganuzi matini ulitumika kusoma na kuchambua vitabu maktabani. Upeo wa utafiti ulikuwa kimuktadha ambapo vitabu vitatu vya fasihi ya Kiswahili vilivyochapishwa mwanzoni mwa milenia mpya katika tanzu tatu za fasihi, yaani riwaya, tamthilia na ushairi, viliteuliwa kutokana na usampulishaji dhamirifu. Jumla ya mashairi kumi na mbili katika Bara Jingine na maonyesho matatu katika Kifo Kisimani yaliteuliwa. Maonyesho haya yalikuwa ni ya kwanza, ya tano na tisa. Katika Babu Alipofufuka, sura ya kumi na nne iliteuliwa kama data ya kimsingi. Uchanganuzi data kithamano ulitumika na maelezo kutolewa kuegemea mihimili ya nadharia. Matokeo yalionyesha kwamba uharibifu wa mazingira ni bayana katika jamii na hili limeangaziwa na watunzi wa Kiswahili. Masuala yaliyobainika ni kama vile uharibifu wa mazingira, sababu za uharibifu wa mazingira, utawala unavyochangia uharibifu wa mazingira na pia athari za uharibifu wa mazingira kwa mtandao wote wa viunga uhai duniani. Pia utafiti ulibainisha kwamba wasanii hawa walipotunga kazi zao, walilenga kuhamasisha jamii, kuzindua binadamu, kutabiri hali ya baadaye na pia kuburudisha jamii kuhusu mazingira yake. Utafiti huu umebaini kuwepo kwa maendeleo ya kisanii katika utunzi wa Kiswahili kwa kuangazia masuala ya kimazingira yanayomsumbua binadamu duniani kote. Hata hivyo, katika kutoa hitimisho utafiti huu umesema kwamba mwanadamu ndiye mdau mkubwa katika mazingira na uwezo wa kuyaokoa au kuyaangamiza zaidi ni wake. Utafiti huu umependekeza kwamba uchunguzi ufanywe zaidi katika fasihi simulizi kwa lengo la kuzua upekee wa kila jamii na tamaduni katika uhifadhi wa mazingira. Utafiti huu utakuwa muhimu katika kuchochea tafiti za baadaye hasa za kimwingiliano-taaluma.