Uchanganuzi kimofosemantiki wa anthroponimu za Kimaragoli zinazojengwa na nomino za kawaida za Kiswahili
Abstract/ Overview
Maana za maneno zinaweza kubadilika kulingana na muktadha wa ufasiri, hali inayoweza kutinga uwasilishaji wa maana ikusudiwayo. Mabadiliko ya kimaana kama haya yanadhihirika pia katika uchunguzi wa anthroponimu za Kimaragoli. Ingawa tafiti zimefanywa kuhusu maana kileksika za anthroponimu za Kimaragoli, vyanzo vya anthroponimu hizo kutokana na nomino za kawaida za Kiswahili, mbinu za kimofolojia zinazounda anthroponimu hizo, pamoja na mabadiliko yake kimaana hazijashughulikiwa. Kutokana na msingi huu, utafiti huu ulichanganua kimofosemantiki anthroponimu za Kimaragoli zilizoundwa kutokana na nomino za kawaida za Kiswahili. Utafiti huu uliongozwa na madhumuni yafuatayo: kuainisha nomino za kawaida za Kiswahili zijengazo anthroponimu za Kimaragoli katika vikoa maana; kufafanua mabadiliko ya kisemantiki katika anthroponimu za Kimaragoli zijengwazo kwa nomino za kawaida za Kiswahili; na kuchanganua mbinu za kimofolojia za uundaji wa anthroponimu za Kimaragoli zijengwazo kwa nomino za kawaida za Kiswahili. Uchunguzi huu uliongozwa na Nadharia ya Pragmatiki Leksia iliyoasisiwa na Blutner (1990). Nadharia hii huchunguza maana ya leksimu kipragmatiki. Kwa kuzingatia muundo wa kimaelezo, utafiti ulifanyika maktabani na nyanjani katika gatuzi Dogo la Sabatia, kaunti ya Vihiga. Usampulishaji dhamirifu ulitumiwa kuteua nomino za kawaida za Kiswahili, watafitiwa, hospitali pamoja na eneo la utafiti. Data ya anthroponimu za Kimaragoli ilikusanywa kutoka kwa baraza la wazee la Wamaragoli pamoja na sajili za majina katika hospitali teule. Data ya utafiti ilikusanywa kwa kutumia mbinu za upekuzi maktabani na usaili usorasmi, na vifaa vya utafiti vilijumuisha orodhahakiki na mwongozo wa usaili. Uhalali, ukubalifu na utegemezi wa data ulithibitishwa na wataalamu wa lugha na jamii ya Wamaragoli. Maadili ya utafiti yalizingatiwa kabla, wakati na baada ya utafiti kwa mujibu wa matakwa ya kibali cha utafiti kutoka MUERC na NACOSTI. Data ilichanganuliwa kimaudhui na kuwasilishwa kimaelezo na katika majedwali. Matokeo ya utafiti yamedhihirisha kuwa nomino za kawaida za Kiswahili zinaweza kuainishwa katika vikoa maana vya wanyama, ndege, vifaa, na mimea. Mabadiliko ya kimaana katika anthroponimu za Kimaragoli zilizojengwa kwa nomino za kawaida za Kiswahili hujumuisha upanuzi, kisio na ubanaji wa maana. Aidha, anthroponimu za Kimaragoli zijengwazo kutokana na nomino za kawaida za Kiswahili huzingatia mbinu za kimofolojia kama vile ukopaji, uhusishaji, uradidi, mwambatanisho na uhulutishaji. Utafiti ulipendekeza tafiti zaidi zifanywe kuhusu mchango wa aina nyingine za nomino pamoja na kategoria zingine za maneno katika ujenzi wa anthroponimu za Kimaragoli na lugha nyinginezo. Matokeo ya utafiti huu yanachangia mijadala ya dhima ya Kiswahili katika kuendeleza misamiati ya lugha nyingine za kiasili, maarifa ya semantiki, mofolojia na onomastiki. Aidha, utafiti huu ni kanzi inayoelimisha kuhusu anthroponimu za Kimaragoli, mabadiliko ya kimaana katika anthroponimu hizo na pia mbinu za kimofolojia zinazozijenga kutokana na nomino za kawaida za Kiswahili.