dc.description.abstract | Kiswahili ni lugha ya Kibantu yenye mifumo na miundo ya kiisimu ambayo ina upekee
wake. Upekee huu husababisha tofauti za kiisimu na lugha nyinginezo za Kibantu kimuundo
na kimfumo na kujenga athari za mwingiliano wa kimofosintaksia unaodhihirika katika
matumizi ya Kiswahili sanifu. Ingawa Kiswahili sanifu kinafundishwa shuleni nchini
Uganda, matokeo ya matumizi yake yanadhihirisha athari za mwingiliano wa miundo na
kanuni za vipashio vya kimofosintaksia vya Luganda katika maandishi na mazungumzo ya
wanafunzi ambao L1 ni Luganda. Azma ya utafiti huu ilikuwa kuchanganua miundo na
kanuni za mofosintaksia za Luganda na Kiswahili ili kubaini athari za mwingiliano wa utafiti
huu ilikuwa: Kwanza, kufafanua jinsi vipashio vya kimofosintaksia vya Luganda sanifu
hufanana na kutofautiana na vya Kiswahili sanifu. Pili, kuchanganua miundo na kanuni za
mifanyiko ya kimofosintaksia ya Luganda na Kiswahili, tatu kutathimini athari za
mwingiliano wa mofosintaksia ya Luganda katika matumizi ya Kiswahili sanifu. Utafiti huu
uliongozwa na mihimili miwili ya Ubia na Upatanifu ya nadharia ya Umilikifu na Unganifu
ya Chomsky (1981). Mihimili ya sarufi bia na upatanifu ilizingatiwa katika kufafanua na
kuchanganua kanuni za mofosintaksia ya Luganda katika Kiswahili sanifu. Muundo wa
kimaelezo ulitumika katika utafiti huu. Utafiti huu ulifanyika katika kata tano za wilaya ya
Kampala, Uganda. Ulijikita katika taaluma ya isimu linganishi na tumikizi. Ulichunguza jinsi
isimu ya lugha za Kibantu huchangiana, kuingiliana na kuathiriana katika matumizi. Mbinu
ya usampulishaji nasibu ilitumika kuteua shule 12 ambazo zinafundisha Kiswahili katika
kidato cha sita. Mbinu ya kimaksudi na dhamirifu ilitumika kuwateuwa wanafunzi 54 wa
kidato cha sita ambao L1 ni Luganda na watumiaji wa Kiswahili kama L2. Data ilikusanywa
maktabani kwa kutumia mbinu ya uchanganuzi matini kutumia kifaa cha kudondoa data cha
orodhahakiki chenye sifa za kimofosintaksia zinazotambulisha vipashio vya kimofosintaksia,
miundo yake na kanuni za matumizi kudodoa data kulingana na malengo matatu ya utafiti.
Nyanjani data ilikusanywa kutoka kwa wanafunzi kupitia kwa mijarabu na mijadala.
Mijadala iliandaliwa kwa wanafunzi kujadili matokeo ya mijarabu ili kutathimini athari za
mwingiliano wa kimofosintaksia wa Luganda katika matumizi ya Kiswahili sanifu katika
maandishi na mazungumzo shiriki. Data ilichanganuliwa na kuwasilishwa kutumia mbinu ya
kimaelezo ikishirikisha majedwali na michoro kudhihirisha jinsi kanuni na miundo ya
mofosintaksia ya Luganda inavyoingiliana na kuathiri matumizi ya Kiswahili sanifu
miongoni mwa wanafunzi wa Kiswahili ambao L1 ni Luganda. Utafiti huu ulibaini kuwa
licha ya Luganda na Kiswahili sanifu kuwa lugha za nasaba moja, ni lugha mbili tofauti za
Kibantu zenye vipashio, miundo na kanuni za mifanyiko ya kimofosintaksia zinazofanana na
kutofautiana. Uchanganuzi ulibaini athari za mwingiliano wa mofosintaksia ya Luganda
katika matumizi ya Kiswahili sanifu. Tathimini ya mwingiliano ulidhihirisha athari za
uhamishaji, ujumlishaji, uchopekaji, udondoshaji, uchanganyaji, uongezaji wa fonimu na
maumbo, miundo na kanuni za mifanyiko ya mofosintaksia ya Luganda katika matumizi ya
Kiswahili sanifu. Athari hizi zilidhihirisha ukiukaji wa matumizi ya maumbo, miundo na
kanuni za vipashio vya kimofosintaksia vya Kiswahili sanifu na kusababisha matumizi ya
Kiswahili kisicho sahihi hasa katika mazungumzo na maandishi ya wanafunzi ambao L1 ni
Luganda. Matokeo haya ni mchango mkubwa katika taaluma ya isimu linganishi ya lugha za
Kibantu kwa kutambua athari za mwingiliano wa vipashio, miundo na kanuni za mifanyiko
ya mofosintaksia ya Luganda kudhihirisha jinsi inavyoathiri matumizi ya Kiswahili sanifu,
kukuza na kuendeleza umilisi na matumizi ya Kiswahili sanifu nchini Uganda. Utafiti huu
ulipendekeza tafiti zaidi kufanywa kuhusiana na mwingiliano wa L1 katika matumizi ya L2
ili kuweka mikakati na misingi ya kukuza na kuendeleza umilisi na matumizi ya Kiswahili
sanifu miongoni mwa wanafunzi unaotokana na mchango na athari za L1. | en_US |