Mwanamke angali tata katika ushairi wa kisasa?
Abstract/ Overview
Sanaa ya ushairi inajisawiri kama nyenzo muhimu katika maendeleo na ukuaji wa binadamu ulimwenguni. Mtunzi wa ushairi hupata ilhamu na tajriba zake kutokana na mitagusana na mivutano ya mijadala ya kimaendeleo inayotokea katika nyakati zake. Uteuzi, uumbaji na uwasilishaji wa sanaa dhamirifu kwa hadhira lengwa ni swala tata sio tu kwa mshairi mbali pia kwa mhakiki. Ujenzi wa taswira zinazowasilisha mada nyeti za kijamii ni changamoto ya kiusanii inayoibua maswala tata. Ndiposa wasilisho hili linachunguza mjadala wa usawiri wa mwanamke katika ushairi wa kisasa. Mada nyingi zinazohakiki matini za kishairi hulenga miuundo, mitindo na maswala mengineyo ya kijamii bila kuangazia swala la utata wa mwanamke. Uzingatifu wa vipengee hivi umefifisha uangafu wa taswira ya mwanamke katika ushairi wa Kiswahili kana kwamba ushairi umempuuza mwanamke kama mhusika mkuu.
Uhakiki huu umechochewa na mjadala aliowahi kuuzwa Said Ahmed Mohamed mwaka wa 1984 katika Kina cha Maisha kwenye Shairi – Mwananamke (uk. 18), lenye kibwagizo “Mwanamke ali tata, tata tulitatulile.” Ni miaka mingi ambayo imepita tangu kuzua swala hili na ndiposa wasilisho hili linatizama utata wa mwanamke katika mashairi (mazingira) ya kisasa. Tahakiki nyingi zinaonyesha kwamba swala la mwanamke katika ushairi liliangazia sana Utenzi wa Mwanakupona ulioandikwa kabla ya karne ya kumi na tisa. Ni dhahiri kwamba katika karne ya ishirini na moja, washairi wengi wameibuka na sanaa na mitindo mbali mbali ambayo inamsawiri mwanamke kwa namna ya kumkweza ama kumtweza kwa matumizi ya jazanda na mitindo mbalimbali ya lugha. Tunatetea kauli kwamba washairi wa kisasa wana nafasi bora ya kumjenga mwanamke kwa njia chanya zaidi hasa ikilinganishwa na washairi awali ambao utamaduni wao ulimtweza mwanamke asemavyo Said Ahmed Mohammed (1984): “Mwanamke ali tunda, ladha yake ili tamu…Mwanamke ali tata tata tuitatulile.” Ni katika muktadha huu ndipo tunachukulia kwamba matini za kishairi za kisasa zinahusisha mbinu na nyenzo mpya ambazo zimebadilisha sura na taswira ya mwanamke. Maswali yanayoibuka ni; Je, Mwanamke angali tata katika ushairi wa kisasa kwenye enzi ya karne ya ishirini na moja? Je, ni kwa kiwango gani washairi wa kisasa wamelitatua swala hili, akiwemo Said Ahmed Mohammed mwenyewe? Je, umbo jipya la mwanamke ni lipi katika ushairi wa kisasa? Katika kujibu maswala ibuka haya uhakiki huu utachunguza ushairi wa Said Ahmed Mohammed, zikiwemo diwani za Jicho la Ndani (2002), Kithaka wa Mberia, Bara Jingine (2001), na mashairi katika Diwani ya Karne Mpya (2007) miongoni mwa nyingine. Ni matumaini yangu kwamba wasilisho hili linatoa mchango mkubwa wa mjengo upya wa taswira ya mwanamke kama nyenzo mojawapo ya kutimiza malengo ya millennia na maono ya 2030.