Mabadiliko katika Umbo la Ushairi na Athari zake katika Ushairi wa Kiswahili
Abstract/ Overview
Mwanadamu amejaribu kwa vyovyote vile kuvumbua na kunyumbua mambo mapya ambayo yataleta mvuto na kupimia akili yake kiubunifu katika hali ya kutaka kutangamana zaidi na binadamu mwenzake au kutaka kuelewa zaidi ulimwengu wake. Ndiposa washairi wengi wa kisasa wanashikilia kwamba ulimwengu unabadilika na hivyo utamaduni wa ushairi lazima ubadilike pia asemavyo Mazrui (1988: viii):
... utamaduni hauna budi kubadilika maadamu uchumi na siasa za nchi zaendelea kubadilika.
Mwelekeo huo unasisitizwa katika mjadala wa Wangari Mwai (1988: 5) anayeonyesha kuwa washairi wa kisasa wanaeleza kwamba fasihi hubadilika katika umbo na maudhui na kwa hivyo ushairi wa Kiswahili sharti uruhusu mabadiliko yanayotokea katika ushairi huru. Katika utangulizi wa swala la “Ushairi, Lugha na Mawazo”(“Poetry, Language and Thought”) Martin Heidegger (1971: xi) anazua swala la tofauti iliyopo kati ya mfikiriaji mshairi na mshairi mfikiriaji; kwamba ili kuwa mshairi mkomavu kuna ufikiriaji ambao mshairi lazima akamilishe. Ufikiriaji ulio na usafi, uzito na umoja wa ushairi. Uwazaji wa kiwango hiki huongezea ubora na utaalamu wa lugha ya ushairi. Fikra kama hizi si za kiajali bali zinakwenda sambamba na ukuaji wa maono ya washairi kwani mshairi alazimika kuzungumzia maudhui ya kiungu, bahari, mawingu, milima, maovu, maafa nk Hiki ni kiwango cha juu cha ufikiriaji na uwazaji unaozungumzia mambo ya kidhahania kuwasilisha uhalisia.