Mifumo ya Kijamii katika Tamthilia Teule za Kiswahili
View/ Open
Publication Date
2020Author
East African Journal of Swahili Studies
Metadata
Show full item recordAbstract/ Overview
Mifumo ya kijamii inajitokeza waziwazi katika fasihi andishi ya Kiswahili. Mifumo hiyo huwakilisha matukio ya fasihi andishi na jinsi yanavyoichora na kwa mapana kuwa kioo cha jamii. Tafiti nyingi zilizofanywa zinahusu vipengele vya fasihi kama vile maudhui, matumizi ya lugha, wahusika na mandhari katika fasihi. Katika tafiti hizo, watafiti hawajaonyesha mifumo jamii inayojitokeza kutokana na vipengele hivi. Utafiti huu umezama na kiutathimini mifumo hii kupitia kwa tamthilia teule za Kiswahili ambazo ni: tamthilia ya Pango (2003) kilichoandikwa na Wamitila, Kifo Kisimani (2008) kilichoandikwa na Kithaka Wa Mberia na Mstahiki Meya (2009) kilichoandikwa na Timothy Arege. Mifumo iliyotafitiwa katika utafiti huu ni: mfumo wa utawala na siasa, wa uchumi katika jamii, wa utamaduni, wa imani na dini, ule wa tabaka za jamii na ule wa elimu ya jamii. Utafiti huu umeongozwa na madhumuni mahsusi yafutayo: kujadili maudhui yanayodhihirisha mifumo ya jamii katika tamthilia teule; kuchanganua mitindo ya lugha inavyodhihirisha mifumo ya kijamii kutoka tamthilia teule; na kuchunguza wahusika katika uhusika wao kwenye mandhari maalumu wanavyojenga ploti inayochangia kuweka wazi mifumo ya kijamii kutoka tamthilia teule. Kiunzi cha nadharia ya uchunguzi kimejengwa na nadharia za uhalisia na nadharia ya umtindo. Mihimili ya nadharia ya uhalisia ikiwemo masuala ya utawala na uongozi, yale ya vijana, udhanifu, ukosefu wa ajira na masuala ya jinsia imebainishwa kadri ilivyojitokeza kupitia tamthilia teule. Mbali na nadharia za uhalisia na umtindo nadharia ya ukoloni mamboleo imetumika kuelezea hali katika tamthilia hasa utambuzi wa mifumo jamii inayotokana na matokeo ya baada ya uhuru. Utafiti umeongozwa na tamthilia 26 zilizoandikwa nchini Kenya na Tanzania tangu mwaka wa 2000. Tamthilia 26 zilizotumika ni zile zilizoandikwa na wazawa asilia wa Afrika Mashariki na kati kufikia mwaka wa 2014. Asilimia kumi ya idadi hiyo ilipeana sampuli ya mbili nukta sita (2.6) ambacho ni kifani tosha cha tamthilia tatu. Utafiti huu umejikita Kenya na Tanzania kwa kigezo kuwa mbali na Kiswahili kuchimbukia na kuenea zaidi katika janibu hizi, imebainika pia kuwa sera na sheria za kikatiba za nchi hizi zimekipa Kiswahili kipao mbele. Orodha ya uchuzaji imetumika kukusanya data. Uchanganuzi wa data ulitumia yaliyomo. Utafiti huu unatarajiwa kuibua mawazo mapya kuhusu mifumo ya kijamii inayotokana na fasihi na hivyo kuchangia katika ukuaji wa elimu.