Uchanganuzi wa kileksikografia wa hiponimia za leksimu nomino na vitenzi vya kiswahili na tafsiri zake katika kiluo
Abstract/ Overview
Ingawa hiponimia hudhihirika miongoni mwa kategoria mbalimbali za maneno, tafiti za Kiswahili zimeelekea kushughulikia hiponimia za nomino na kupuuza kategoria nyingine kama vile vitenzi, vielezi na vivumishi. Tafiti hizi zimefanywa pia bila kuhusisha mitazamo ya kiisimu ya uainishaji na nadharia faafu zingativu. Aidha, hakuna tafiti za kimuundo na kimtindo kuhusu hiponimia zilizofanywa baina ya Kiswahili na lugha nyingine za Kiafrika. Hivyo basi, utafiti huu ulihusisha uchanganuzi wa kileksikografia wa hiponimia za leksimu nomino na vitenzi vya Kiswahili na tafsiri zake katika Kiluo kwa minajili ya kuimarisha tafiti zao linganishi za kimuundo na kimtindo. Madhumuni yafuatayo yalizingatiwa: kuchanganua kileksikografia na kuainisha hiponimia za leksimu nomino na vitenzi vya Kiswahili, kutafsiri kiisimu hiponimia za nomino na vitenzi vya Kiswahili katika Kiluo, na kulinganisha na kulinganua kimuundo na kimtindo hiponimia za nomino na vitenzi vya Kiswahili na Kiluo. Utafiti huu uliongozwa na mseto wa nadharia ya uchanganuzi vijenzi ya Katz na Fodor ya kuchanganua vijenzi vya maana kileksika kwa kuzingatia sifa bainifu iliyotumiwa kuainisha hiponimia za Kiswahili, na nadharia ya tafsiri kwa mujibu wa Catford iliyotumiwa kutafsiri hiponimia za Kiswahili katika Kiluo. Utafiti huu ulihusisha uchanganuzi wa hiponimia za nomino na vitenzi vya Kiswahili kutoka KK21 na KKS na visawe vyake katika Kiluo kutoka EDD na DED. Muundo kimaelezo unaohusisha maelezo na uchanganuzi data katika majedwali ya solo ulizingatiwa. Utafiti huu ulifanyika maktabani na nyanjani katika kaunti ndogo ya Kisumu Mashariki. Usampulishaji dhamirifu ulitumiwa kuteua wasailiwa Waluo 35, na pia hipanimu kuu 28 za nomino na 24 za vitenzi zilizochanganuliwa hadi kufikia kiwango kifu. Mbinu za upekuzi na usaili muundo usorasmi zilitumiwa kukusanya data huku modeli ya uhusiano wa leksikoni kisintaksia na dodoso zikitumiwa kama vifaa. Data husika ziliyakinishwa kwa kutumia mtindo wa uthibitishwaji, kuchanganuliwa kimaudhui na katika majedwali ya solo, na hatimaye kuwasilishwa kileksikografia. Utafiti huu ulibainisha kuwa hiponimia za leksimu za Kiswahili huweza kuchanganuliwa kileksikografia na kuainishwa kimaudhui katika mikondo sita kama vile kitambuzi, kidhanishi au kiuamilifu, kijiografia, kitukio, kihali na kitendo.Visawe linganifu na kapa hudhihirika katika tafsiri ya hiponimia za Kiswahili katika Kiluo. Miundo na mitindo ya hiponimia hulingana na kutofautiana katika uchanganuzi wa hiponimia kiuamilifu kwa sababu ya tofauti za kijiografia na kitamaduni za lugha hizi mbili. Matokeo yake ni mchango mkubwa katika taaluma za semantiki kileksika na tafsiri, mafunzo ya misamiati ya Kiswahili na Kiluo, na kudhukuriwa kama makala kivo ya leksikografia thaniya ya Kiswahili na Kiluo, na kama matini ya thesauri sahili iliyotafsiriwa ya lugha hizi mbili.