Show simple item record

dc.contributor.authorKARUHANGA, Deusdedit
dc.date.accessioned2026-02-17T06:48:32Z
dc.date.available2026-02-17T06:48:32Z
dc.date.issued2025
dc.identifier.urihttps://repository.maseno.ac.ke/handle/123456789/6430
dc.descriptionPhD Thesisen_US
dc.description.abstractKatika mfumo wa elimu nchini Uganda, Kiswahili ni lugha muhimu kwa mawasiliano na maendeleo ya kijamii. Hata hivyo, wanafunzi wanaozungumza Runyakitara wanakabiliwa na changamoto mbalimbali katika ujifunzaji wa Kiswahili, hasa katika matumizi ya vivumishi. Changamoto hizi zinatokana na tofauti za kimuundo na kimaana baina ya vivumishi vya Runyakitara na vivumishi vya Kiswahili, hali inayopelekea makosa ya kiisimu katika mchakato wa ujifunzaji. Wanafunzi ambao lugha yao ya kwanza (L1) ni Runyakitara moja ya lugha za Kibantu zinazoenea Kusini Magharibi mwa Uganda, hukumbana na changamoto mahsusi wanapojifunza Kiswahili kama lugha ya pili (L2). Kwa hivyo, utafiti huu ulichunguza athari za vivumishi vya Runyakitara katika ujifunzaji wa Kiswahili.Utafiti huu uliongozwa na malengo maalum: Kubainisha tofauti za kimuundo kati ya vivumishi vya Runyakitara na Kiswahili, Kuchunguza athari za vivumishi vya Runyakitara katika ujifunzaji wa Kiswahili, na Kutathimini makosa ya kiisimu yanayotokana na uhamishaji wa vivumishi vya Runyakitara kwenye ujifunzaji wa Kiswahili. Utafiti huu uliongozwa na Nadharia ya Uchanganuzi Linganuzi (contrastive analysis), ambayo ilianzishwa awali na Fries, Weinreich, Haugen, na Lado (1950), kisha ikaendelezwa na James (1980) na Jean (2022). Mihimili muhimu ya nadharia hii iliyotumiwa ni: mfanano na tofauti za lugha, uingiliaji wa lugha ya kwanza (L1), uhamishaji chanya na hasi, na utambulisho wa makosa. Nadharia hii ilitumika kuchanganua athari za vivumishi vya Runyakitara katika ujifunzaji wa Kiswahili sanifu. Muundo wa kimaelezo ulitumika katika utafiti huu, ambao ulifanyika katika Jiji la Mbarara, Uganda, ukilenga taaluma ya isimu linganishi. Idadi lengwa ya utafiti ilikuwa wanafunzi 100 wanaosoma Kiswahili katika shule 10 za sekondari jijini Mbarara. Washiriki hawa waliteuliwa kwa kutumia mbinu mseto: usampulishaji wa nasibu ulitumiwa kutambua shule10 zinazofundisha Kiswahili na usampulishaji wa kimaksudi ulitumiwa kuteua wanafunzi ambao lugha yao ya kwanza ni Runyakitara kutoka kwenye shule hizo na vitabu vya sarufi vya Runyakitara na Kiswahili. Data ya nyanjani ilikusanywa kwa kutumia mjarabu wa kimaandishi na mjarabu wa kimazungumzo kutoka kwa wanafunzi, huku data ya maktabani ikipatikana kupitia uchambuzi wa matini kwenye vitabu vya sarufi vya Runyakitara na Kiswahili. Zana zilizotumika ni Kifaa cha Mijarabu ya Kiisimu, kifaa cha kinasa sauti, kifaa cha orodha ya uchunguzaji wa miundo ya vivumishi yenye sifa za Kimofolojia. Data iliyokusanywa ilichanganuliwa na kuwasilishwa kwa mbinu ya kimaelezo, ikishirikisha majedwali na michoro ili kuonyesha miundo, athari, na makosa ya kiisimu ya vivumishi vya Runyakitara katika ujifunzaji wa Kiswahili. Matokeo ya utafiti yalilingana na malengo yake matatu: ilionekana kwamba vivumishi vya Runyakitara na Kiswahili vinafanana katika baadhi ya vipengele vya kimofolojia lakini hutofautiana kimsingi katika upatanishi wa kisarufi na mpangilio wa maneno. Pili, vivumishi vya Runyakitara huathiri ujifunzaji wa Kiswahili kwa kuhamishwa moja kwa moja, na kusababisha makosa ya kimuundo na kisintaksia, tatu, makosa ya mwanafunzi yalibainika zaidi katika uhusishaji wa kivumishi na nomino, matumizi ya viambajengo vya kivumishi, na mfuatano wa vivumishi. Kwa hivyo, utafiti ulibaini kuwa ingawa Runyakitara na Kiswahili ni lugha za nasaba moja ya Kibantu, tofauti za kimuundo na matumizi ya vivumishi zinawapa wanafunzi changamoto kubwa katika kujipatia Kiswahili L2. Utafiti huu unahimiza maendeleo ya mbinu bora za ujifundishaji lugha, unasaidia watunga mitaala kuelewa mapungufu ya wanafunzi, na unapanua mijadala ya kitaaluma kuhusu ujifunzaji wa lugha ya pili kwa muktadha wa lugha zinazokaribiana.en_US
dc.publisherMaseno Universityen_US
dc.titleAthari ya vivumishi vya Runyakitara kwa ujifunzaji wa kiswahili katika shule za upili jijini Mbarara, Ugandaen_US
dc.typeThesisen_US


Files in this item

Thumbnail

This item appears in the following Collection(s)

Show simple item record