| dc.description.abstract | Upekee katika uundaji wa kazi ya fasihi huitwa mtindo na hutofautiana kutoka mwandishi mmoja hadi mwingine. Mtunzi huweza kuchagua mtindo wa kueleza kazi yake unaodhihirika sio tu ndani mwa kazi hiyo bali pia kupitia jalada la kitabu kama vile jalada la mbele na la nyuma. Kimsingi, jalada huwa na mawasilisho kama vile rangi na picha zinazowasilisha maudhui yaliyomo katika kazi husika ya fasihi. Wahakiki wengi wana mazoea ya kuchambua majalada hayo kwa kutaja tu rangi na picha zinazodhihirika na kuzihusisha na matukio yaliyomo kitabuni moja kwa moja bila kuzingatia nadharia yoyote. Wengine huzingatia jalada la mbele tu katika uchambuzi wao na kupuuza lile la nyuma lililo na blabu iliyo na mtindo wake wa kimuundo na kiisimu. Utafiti huu ulifanywa kwa lengo kuu la kuchunguza matumizi ya jalada kama mtindo katika kuakisi maudhui katika riwaya ya Utengano (Mohammed, 2009) na Chozi La Heri (Matei, 2014). Utafiti uliongozwa na madhumuni matatu; kubainisha rangi na picha katika majalada kama mtindo wa kuakisi maudhui katika riwaya ya Utengano (Mohammed, 2009) na Chozi La Heri (Matei, 2014), kuchambua maudhui yanayowasilishwa na rangi na picha katika majalada kama mtindo wa kuakisi maudhui katika riwaya ya Utengano (Mohammed, 2009) na Chozi La Heri (Matei, 2014) na kuhakiki vipashio vinavyojenga blabu kama mtindo wa kuakisi maudhui katika riwaya ya Utengano (Mohammed, 2009) na Chozi La Heri (Matei, 2014). Utafiti uliongozwa na nadharia ya Semiotiki kwa mujibu wa Peirce na kuendelezwa na Ferdinand, Barthes, Wamitila na Massamba, na pia nadharia ya Muundo Kipera kwa mujibu wa Swales. Kimsingi Semiotiki hutazama ishara za matini zinavyofungamanishwa na maana kifasihi. Nadharia hii ilitumiwa kuchambua namna rangi na picha zilizopo kwenye majalada zinavyoingiliana na matukio katika riwaya ya Utengano (Mohammed, 2009) na Chozi La Heri (Matei, 2014). Nadharia ya Muundo Kipera hushughulika na vipashio vinavyopatikana katika uandishi wa blabu, ikiwemo hatua za uandishi na mshikamano. Utafiti ulizingatia muundo kiuchanganuzi. Eneo la utafiti lilikuwa la kithematiki ya umitindo na kiisimu katika fasihi. Usampulishaji maksudi ulitumika ambapo sampuli mbili, riwaya ya Utengano (Mohammed, 2009) na Chozi La Heri (Matei, 2014) ziliteuliwa. Data kutoka kwenye riwaya ilikusanywa kupitia mbinu ya unukuzi. Orodha ya uhakiki ilitumika kama kifaa. Uchanganuzi wa data ulifanywa kimaudhui na kuwasilishwa kwa maelezo ya kinathari. Matokeo ya utafiti yalibainisha rangi kama vile nyeupe, nyeusi, nyekundu, kijani kibichi, manjano, samawati na hudhurungi. Picha zilizobainishwa katika Utengano (Mohammed, 2009) ni kama vile mwanamke aliyevalia buibui, kasri, bahari na nyumba ya matope na mabati. Katika Chozi la Heri (Matei, 2014) kuna picha ya jicho linalodondoka chozi ambamo kuna vijana watatu wanaoukumbatiana. Maudhui kutokana na rangi na picha ni kama vile ukahaba, ufisadi, ukoloni mamboleo, utengano, mapenzi, ndoa na nafasi ya mwanamke. Aidha, matokeo yalidhihirisha misogeo hatua minne ya uandishi wa blabu katika riwaya zote mbili; maelezo au utangulizi, kuhusu mwandishi, kampuni ya uchapishaji na maudhui kutoka kitabuni. Maudhui kutokana na misogeo hatua ni utengano, mabadiliko, tamaa na ukabila. Vipengele vya mshikamano kama vile urejeshi, uunganishaji, udondoshaji ubadilishaji na hiponimu vilibainishwa. Utafiti huu utasaidia katika uchambuzi wa majalada ya kazi mbalimbali za fasihi ya Kiswahili kinadharia. Aidha, utasaidia wahakiki wa fasihi, wakuza mitaala na kampuni za uchapishaji kuzingatia zaidi uboreshaji wa majalada ili kuvutia makini ya wasomaji. | en_US |