dc.description.abstract | Lugha ni chombo maalum katika ustawishaji na uimarishaji wa rasilimali za mwanadamu. Pia, ni wenzo unaohimili sera ambazo hulenga katika kutimiza matarajio ya kitaifa katika nchi yoyote ile. Nchini Kenya, vipengele katika katiba ya 2010, vinavyohusu lugha vilipandisha hadhi lugha ya Kiswahili ili iweze kutumika kama lugha ya taifa na rasmi sambamba na Kiingereza. Hata hivyo, katiba hii haijaweka kanuni zinazolenga kuimarisha na kudumisha uanuwai wa lugha za kiasili kote nchini Kenya. Machukulio ni kwamba, vipengele vya katiba vinasheheni sifa stahilifu kama vile, usawa wa kimatumizi, utekelezwaji, mikao ya kieneo, matakwa, pamoja na hiari za wananchi. Kwa kuangazia hali ya kiisimu-jamii katika Kaunti ya Bungoma, utata upo katika udumishaji wa mfumo ‘rasmi’ wa sera ya lugha Kitaifa, na utekelezwaji wa sera ya lugha kupitia asasi za serikali na zile za umma. Kazi hii inalenga kuchanganua uamilifu wa Kiswahili na Kibukusu kupitia ruwaza zinazodhihirika katika mawanda mbalimbali ya lugha katika Kaunti ya Bungoma. Mihimili ya nadharia ya sera ya lugha iliyoendelezwa na Spolsky (2004, 2007) ambayo ni Usimamizi wa lugha na Ikolojia ya lugha pamoja na ruwaza za lugha ilivyoelezwa na Paltridge (2001) ndiyo nguzo ya kuchanganua utafiti huu. Aidha, mtazamo wa Haugen (1972) unaohusu Ikolojia ya lugha umetumika katika kudhihirisha michakato baina ya lugha na mazingira inamotumika. Muundo mseto uliojumuisha, muundo wa kimaelezo, kiupelelezi na wa kiiktisadi ulitumiwa. Usampulishaji dhamirifu ulitumiwa kuteua matumizi ya lugha ya KS, KB na KS/KB katika ruwaza za lugha zilizodhihirika katika mawanda ya biashara, kanisani na utawala hasa kwenye mikutano ya umma au baraza za Chifu katika maeneo mbalimbali ya Kaunti ya Bungoma. Data ilikusanywa kwa kutumia mbinu ya uchunzaji usio-shirikishi na ya kiiktisadi ilikusanywa kwa kuhesabu hali ambazo lugha za KS, KB au KS/KB zilitumiwa. Ilibainika kuwa lugha ya KS na KB hukamilishana kiuamilifu katika mawanda mbalimbali ya kijamii katika Kaunti ya Bungoma. | en_US |