dc.description.abstract | Umilisi wa lugha ya kifasihi kutokana na fasihi andishi ya Kiswahili ni uti wa mgongo kwa ufanisi wa mtihani wa Kiswahili. Wanafunzi wanapoanza kidato cha kwanza huwa wamepata alama nzuri katika mtihani wa Kiswahili. Mtaala na mtihani katika hiki kiwango hauhusishi umilisi wa lugha ya kifasihi kutokana na vitabu vya fasihi andishi vilivyoteuliwa. Kwa hivyo, wanafunzi huanza kidato cha kwanza kabla hawajatangulizwa katika umilisi wa lugha ya kifasihi unaotokana na fasihi andishi. Ukosefu wa utangulizi wa lugha ya kifasihi kabla ya kujiunga na kidato cha kwanza huzua pengo la umilisi wa lugha ya kifasihi. Hii ni kwa sababu punde baada ya kujiunga na shule za upili, wanafunzi wa kidato cha pili hutahiniwa katika vipengee vya lugha ya kifasihi, ambapo hawana umilisi wa lugha ya kifasihi wa kukabiliana na hiyo mitihani. Hali hii huzua msingi dhaifu wa kuipasi mitihani ya kieneo na kitaifa katika kidato cha nne. Ufanisi wa matokeo ya mitihani kabla ya kuhusishwa na lugha ya kifasihi, na udhaifu wa matokeo baada ya kidato cha kwanza, ni hali iliyochochea na kufungua mwanya wa swala la utafiti huu, ambao ulichunguza umilisi wa lugha ya kifasihi miongoni mwa wanafunzi wa shule za upili katika kaunti ndogo ya Wareng’, kaunti ya Uasin Gishu. Madhumuni ya utafiti ni: Kuchunguza vigezo vya umilisi wa lugha ya kifasihi vya fasihi andishi ya Kiswahili ambavyo wanafunzi wanao hitimu kidato cha pili wanavitumia ili kutatua tatizo la pengo la umilisi wa lugha hiyo. Kupambanua mikakati ya kiuamalifu na kimakusudi ambayo wanafunzi kufikia kidato cha pili wameitumia ili waweze kusoma vitabu vya fasihi andishi ya Kiswahili vilivyoteuliwa na Taasisi ya kukuza Mitaala Nchini. Kudadavua mfanano na tofauti za umilisi wa lugha ya kifasihi kati ya wanafunzi wa kidato cha nne na kidato cha pili kiulinganishi. Kubainisha iwapo kufikia kidato cha nne wanafunzi walihusishwa na mikakati ya mtaala shirikishi nje ya mtaala rasmi ili kukuza umilisi wa lugha ya kifasihi. Nadharia ya Uamalifu, iliyoasisiwa na John Dewey (1952) na kuendelezwa baadaye na Tomasello (20000) ilitumiwa. Mihimili iliyouongoza utafiti ni: Mwanafasihi huhitaji umahiri wa kufafanua maana za dhana za kiusomi katika matumizi ya kila siku; wazo na maelezo ya kiusomi yaonyeshwe kwa njia ya utendaji; Umilisi wa lugha sio tukio funge la wakati mmoja; Umilisi wa lugha unaweza kupatikana nje ya darasa rasmi. Nadharia hii iliongoza utafiti kubainisha kwamba stadi za lugha zinaweza kutumiwa kiuamalifu ili kuibua umilisi wa kinachosomwa kwa ufanisi mkuu. Muundo wa utafiti wa kisifa ulizingatiwa. Utafiti uliendelezwa katika kaunti ndogo ya Wareng’. Kithematiki utafiti ulijikita katika matumizi ya lugha ya kifasihi katika fasihi andishi kwa wanafunzi wa sekondari. Kundi lengwa lilikuwa wanafunzi wa kidato cha pili na kidato cha nne wanaofanya mitihani ya Kiswahili Wareng’, ambao walikuwa jumla ya 3873. Usampulishaji ulihusisha: Shule 12 za kiwango cha Kaunti ndogo; walimu 12 wa Kiswahili; na mtaalamu mmoja mmoja kutoka Taasisi ya Kukuza Mitaala Nchini na Baraza la Mitihani la Kitaifa la Kenya. Idadi ya shule 12 ilisampulishwa kinasibu kama thuluthi moja ya shule zote 38 zilizokuwa zimesajiliwa. Kati ya kundi lengwa ya 3873 kutoka kidato cha nne na cha pili, sampuli ilikuwa 2073 kutoka kidato cha pili na 1800 kutoka kidato cha nne. 2073 ilipimwa kwa asilimia 11% ili kupata sampuli ya 230; 1800 ilipimwa vivyo hivyo kwa mujibu wa wataalamu na kupata sampuli ya 200. Mbinu za kukusanya data zilikuwa uchunzaji darasani, usaili, upekuzi, dodoso na hojaji. Vifaa vilivyotumiwa ni mwongozo wa orodha ya uchunzaji, hojaji, maktaba na matini za kifasihi. Data ilichanganuliwa na kuwasilishwa kiwingi idadi na kisifa. Utafiti uliwekwa katika sura tano. Matokeo yalionyesha kwamba wanafunzi wa shule za upili katika kaunti ndogo ya Wareng’ wana kiwango cha chini cha umilisi wa lugha ya kifasihi, kwa hivyo walihitaji kuhusishwa katika kuisoma fasihi andishi ili wapate umilisi wa lugha ya kifasihi kwa manufaa ya ufanisi. Umuhimu wa utafiti huu ni pamoja na kuonyehsa ubora wa kuwahusisha wanafunzi wa shule za upili katika umilisi wa lugha ya kifasihi kama kiungo muhimu kwa ufanisi; kuongezea maarifa ya kiusomi, na kuonyesha nafasi ya stadi za lugha katika kujenga umilisi wa lugha ya kifasihi. | en_US |