dc.description.abstract | Biblia takatifu inayo misingi yake mikuu katika tamaduni za Wayahudi, yaani ni mkusanyiko wa vitabu vyenye maumbo ya fasihi simulizi. Ingawa kumekuwa na tafiti anuai kuhusu maumbo ya fasihi simulizi, chache zimefanywa kuhusu mwingiliano matini wa maumbo ya fasihi simulizi katika Biblia. Utafiti huu ulidhamiria kutathmini maumbo ya fasihi simulizi katika vitabu teule vya Biblia ili kuziba hili pengo. Utafiti huu ulilenga kuhakiki mwingiliano matini kati ya fasihi simulizi na Biblia. Madhumuni ya utafiti huu yalikuwa: kuchanganua maumbo ya fasihi simulizi katika matini teule katika Biblia; kupambanua mwingiliano matini wa fasihi simulizi na matini teule ya Biblia; kutathmini mchango wa Biblia katika ukuzaji wa fasihi simulizi. Upeo wa utafiti huu ni maumbo ya fasihi simulizi katika vitabu saba vya Biblia ya Tafsiri Jipya la Kimataifa; kitabu cha Mwanzo, Wafalme wa kwanza na Wafalme wa pili, Zaburi, Mithali, Mathayo na Luka. Nadharia iliyoongoza utafiti huu ni nadharia ya mwingiliano matini iliyoasisiwa na Julia Kristeva mwaka wa 1969. Mihimili mitatu ya nadharia hii ni; kazi za kifasihi huingiliana na kuhusiana; matini hupeana umatini ambamo matini nyingine zinaweza kuundwa na kufasiriwa; fasihi hutokana na fasihi. Muundo wa kimaelezo ulizingatiwa. Ili kupata sampuli yenye sifa zifaazo, usampulishaji dhamirifu ulitumiwa. Data ilikusanywa maktabani kwa kusoma na kudondoa maumbo ya fasihi simulizi yaliyoafiki madhumuni ya utafiti kwa kutumia orodha ya uchunzaji. Uchanganuzi wa yaliyomo ulifanywa. Data iliwasilishwa kwa njia ya maelezo nayo matokeo yakafasiriwa kuzingatia swala la utafiti, mihimili ya nadharia na madhumuni ya utafiti. Matokeo ya utafiti huu yalikuwa ifuatavyo; kwanza, maumbo manne makuu ya fasihi simulizi yalidhihirika katika vitabu vilivyoteuliwa; pili, ilibainika kwamba fasihi simulizi huingiliana na matini teule ya Biblia; tatu, Biblia ina mchango mkubwa katika fasihi simulizi hivyo husaidia katika ukuzaji na uhifadhi wake. Utafiti ulihitimisha kuwa kuna mwingiliano matini kati ya fasihi simulizi na matini teule za Biblia. Mwingiliano huu ulidhihirika kutokana na jinsi maumbo ya fasihi simulizi yalivyoingiliana na matini teule za Biblia. Utafiti unatarajiwa kupanua uwanja wa fasihi simulizi kwa kukuza swala la mwingiliano matini. Utafiti unapendekeza kuwa Biblia itumiwe kama rejea ya maumbo ya fasihi simulizi. Hii itachochea wasomi wa fasihi simulizi na watafiti wa baadaye kusoma Biblia kama kitabu cha fasihi simulizi, hasa wanapochanganua maumbo ya fasihi simulizi. | en_US |